KUWA MAKINI SANA UNAMWAMINI NANI.

By Pastor Carlos.
"Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hata katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hata akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake."  (2 SAM. 3:26-27 SUV).
Abneri alikufa kipumbavu sana mikononi mwa Yoabu kwa sababu alimwamini mno Yoabu asijue kuwa nia ya ndani ya Yoabu ilikuwa ni kumwangamiza. Moyo wa Asaheli ulikuwa sahihi ila wa Yoabu haukuwa sahihi. Asaheli alijiaminisha kwa mtu hatari sana ambaye baadaye akawa ndo sababu ya kufa kwake. Alikubali kwenda faragha kusema naye wakati nia ya Yoabu ni kutumia hiyo faragha kummaliza Asaheli.


Ni wale wale ambao tunawaamini faraghani ndo wanatuua hadharani kesho. Kuwa makini sana unamwamini nani. Mtu yule yule ambaye Asaheli alimwamini ndiye aliyemchoma na mkuki na pamoja na kwamba Asaheli alikuwa shujaa sana na mpiganaji hodari, alipomwamini Yoabu hakuchukua tahadhari stahiki dhidi ya Yoabu ikampa Yoabu nafasi (tactical advantage) dhidi yake akammaliza na kumwuua.

Wakati Daudi anamwombolezea Asaheli sikia maneno ya Daudi:
"Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia." (2 SAM. 3:33-34 SUV).

Asaheli hakufa kipumbavu kwa sababu hakuwa na namna ya kuzuia hicho kifo bali kwa sababu alimwamini mtu asiyestahili kabisa kuaminiwa. Kuwa makini sana unamwamini nani.
Asaheli alimwamini Yoabu kwa moyo safi ila Yoabu hakustahil kabisa kule kuaminiwa maana alitumia kule kuaminiwa kinyume cha Asaheli tena kwa kumdhuru na kumwangamiza Asaheli.
Amasa naye alikufa kifo cha kijinga vile vile mikononi mwa Yoabu.

"Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akiendelea, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao wa tumbo, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri." (2 SAM. 20:8-10 SUV).
Yoabu alitumia mbinu ile ile aliyoitumia dhidi ya Asaheli kummaliza Amasa. Alitumia kule Amasa kumwamini kama mbinu ya kivita (tactical advantage) dhidi ya Amasa. Alimsemesha Amasa kwa maneno sahihi ila Amasa hakuona kilichokuwa mkononi mwa Yoabu kama ambavyo huwa sisi tunadanganyika kirahisi na maneno matamu na ya amani ya watu bila kujua walichobeba mioyoni mwao.
Yoabu akajifanya kama anamkumbatia Amasa na kwa kuwa Amasa hakuwa na sababu ya msingi ya kutomwamini Yoabu hakuchukua tahadhari ipasayo dhidi ya Yoabu na akateremsha ulinzi na kinga dhidi yake akafa kwa kosa hilo la kiufundi. Amasa alimwamini Yoabu ila Yoabu hakustahili kule kuaminiwa maana alitumia kule kuaminiwa dhidi yake Amasa akamwua. Kuwa makini sana unamwamini nani.
Yesu Naye alisalitiwa na kuwekwa mikononi mwa adui Zake na mtu wa ndani aliyemwamini sana yaani Yuda. Tena alimwamini Yuda maka akamfanya mweka hazina wake lakini Yuda huyo huyo akamsaliti Yesu mikononi mwa adui Zake. Alitumia kule kujua taarifa za ndani kummaliza Yesu.
"Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu. Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu" (LK. 22:47-48 SUV). Hata Yuda hakumsaliti Yesu kama adui Yake bali kama rafiki Yake.
Maneno Yesu aliyouliza sio maneno mepesi hata kidogo. Anamuuliza Yuda, ".... unamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?"
Yaani ni kama anamwambia nilikuamini alafu unatumia kule mimi kukuamini kinyume nami kunisaliti kwa adui zangu? Hili lazima lilimwuumiza Yesu kuliko tendo lile la kuangukia mikononi mwa wale askari maana alijua wazi kuwa lazima aende tu msalabani lakini njia aliyoiendea ilimwumiza sana Yesu.
Yuda aliaminiwa akawa moja ya watu wa ndani sana aliyeyajua mambo ya ndani sana lakini Yuda hakustahili kule kuaminiwa akatumia hizo taarifa za ndani kumsaliti Yesu kwa adui Zake. Kuwa makini sana unamwamini nani maana unaweza ukamwamini mtu ambaye akatumia taarifa za ndani ulizomwamini nazo kukusaliti na kukuangamiza kwa adui zako. Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.  (MIT. 27:6 SUV).
Wengi wetu tunawaepuka marafiki ambao wanatuambia ukweli na kuwa karibu na maadui ambao wanaonekana machoni petu wanasema nasi maneno matamu ya kutujali bali wakitoka mbele yetu wanaenda kuturarua na kutusaliti kwa maadui zetu.
Mara nyingi maadui wa hatima yako watakubusu sana. Watakusemesha sana kwa maneno matamu ili kukufanya usiwashuku wala kuwadhania na kuteremsha ulinzi wako dhidi yao. Hilo ndo kosa ambalo alilifanya Abneri na Amasa. Walimwamini mno Yoabu na hawakuchukua tahadhari yoyote dhidi yake. Hawakujilinda wala kujikinga dhidi yake maana walimwamini kama rafiki wakati kwa kweli huyu mtu alikuwa hatari sana na baadaye alikuja kuwaua. Abneri na Amasa walikufa kijinga sana mikononi mwa mtu ambaye walimwamini wakati hakustahili kabisa kuaminiwa nao maana hakuwa na moyo sahihi.
Maandiko yanasema: "Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari." (MIK. 7:5 SUV).
Kuwa makini unamwamini nani na nini? Itakuepusha na maumivu mengi yasiyo na sababu kwenye safari ya kuelekea hatima yako.

0 comments:

Post a Comment